Skip to main content

Mwaka watimia tangu tetemeko kubwa la ardhi Nepal

Mwaka watimia tangu tetemeko kubwa la ardhi Nepal

Mwaka mmoja tangu mfululizo wa matetemeko makubwa ya ardhi nchini Nepal, shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP na wadau wake wanaendelea kusaidia harakati za nchi hiyo iweze kujikwamua kwa uendelevu kutoka janga hilo.

Matetemeko hayo yaliua watu zaidi ya 8,700 huku zaidi ya Elfu 22 wakijeruhiwa ilhali miundombinu muhimu kama vile majengo na njia za waenda miguu zitumiwazo na watalii kupanda milimani ziliharibiwa.

UNEP inasema maporomoko ya udongo yalitwamisha maji na hata mito kuzuiwa na udongo huku mingine ikibadilisha mwelekeo wao na hivyo kusababisha baadhi ya watu kukosa huduma ya maji.

Gharama ya kiuchumi kutokana na matetemeko hayo ya ardhi kuharibu mifumo anuai imekadiriwa kuwa dola Milioni 328.

 

image
Watoto wakiwa kwenye moja ya mahema ambayo ni makazi. (Picha:© UNICEF Nepal/2016/Mathema)
Nalo shirika la afya duniani WHO limesema matetemeko hayo ya ardhi ni fundisho la jinsi la kujiandaa dhidi ya majanga ya asili yanayoweza kutokea siku za usoni.

 Mkurugenzi wa WHO kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia Dkt. Poonam Khetrapal Singh amesema hayo akihutubia mkutano wa siku mbili wa kujifunga kutokana na tetemeko la ardhi Nepal mwaka 2015.

Wakati huo huo Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupunguza athari za majanga Robert Glasser, ametoa wito kwa uwekezaji zaidi iwapo nchi zinataka kupunguza idadi ya wahanga watokanao na matetekeno ya ardhi.

Amesema tetemeko la ardhi Nepal la 7.8 katika kipimo cha richa, lilitarajiwa na hivyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi siku za usoni.

image
Harakati za ukarabati milimani baada ya tetemeko la ardhi, Nepal. (Picha:: UNEP GRID Arendal/Lawrence Hislop)
Bwana Glasser amesema jitihada za ujenzi mpya wa Nepal zikiendelea, usaidizi zaidi unatakiwa kwa watu Milioni Tatu au zaidi ambao walipoteza makazi yao na usaidizi huo wa ujenzi uzingatie viwango ili majengo yaweze kustahimili mitetemo.