Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC kuanza kufanya tathmini ya awali kuhusu hali nchini Burundi

ICC kuanza kufanya tathmini ya awali kuhusu hali nchini Burundi

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Fatou Bensouda, ametangaza kwamba ameamua kufanya tathmini ya awali kuhusu hali nchini Burundi tangu mwezi Aprili 2015. Taarifa kamili na Joseph Msami..

(Taarifa ya Msami)

Akitangaza uamuzi huo, Bi Fatou Bensouda amesema kuwa amekuwa akifuatilia hali nchini Burundi tangu mwezi Aprili 2015, akitoa wito wa mara kwa mara kwa pande zote zijiepushe na ukatili, na kuonya kuwa wanaotenda uhalifu unaotambuliwa chini ya mamlaka ya ICC watawajibishwa Kama watu binafsi.

Amesema tathmini ya awali siyo uchunguzi, lakini ni mchakato wa kufanyia tathmini taarifa zilizopo ili kuamua iwapo vigezo vya kuanza kufanya uchunguzi vimetimizwa, kulingana na Mkataba wa Roma.

(Sauti ya Fatou Bensouda)

“Burundi ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma. Hii inamaanisha ICC ina mamlaka juu ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliotekelezwa ndani ya mipaka yake au na raia wa Burundi tangu Disemba mosi 2004. Ikipatikana kuwa uhalifu kama huo huenda umetekelezwa dhidi ya waathirika wa Burundi, ni jukumu langu la kisheria kuchukua hatua chini ya Mkataba wa Roma.”

Katika mzozo unaoendelea nchini Burundi, zaidi ya watu 430 wameripotiwa kuuawa, huku watu wapatao 3,400 wakiwa wamekamatwa, na zaidi ya 230,000 kulazimika kuhama makwao.