Zimbawe, Rwanda zaangazia hatua baada ya kutia saini #MkatabawaParis

22 Aprili 2016

Viongozi mbali mbali walioshiriki katika utiaji saini mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wamepata fursa pia ya kuhutubia na kuelezea kile ambacho wanatarajia kufanya baada ya kazi hiyo adhimu.

Miongoni mwao ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye pamoja na kusema nchi yake itachukua hatua haraka kuridhia mkatab huo, amefananisha na vita harakati za kukabili mabadiliko ya tabianchi hivyo akasema..

“Mkataba wa Paris na saini zetu ambazo tumeweka mapema leo vinathibitisha kuwa hatua bora na za pamoja zinazotambua mazingira ya kila nchi zetu ni sharti la kufanikiwa katika vita hivi. Tunatarajia nchi zilizoendelea zichukue nafasi yao ya uongozi kama zinavyowajibishwa na mkataba wa Paris kwenye hatua hizo.”

image
Louise Mushikiwabo, Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda akitia saini mkataba wa PAris. (Picha:UN/Susan Markisz)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo akapata fursa ya kuhutubia akaeleza hatua ambazo wamechukua ikiwemo kupiga marufuku mifuko ya plastiki. Amesema hata hivyo safari bado ni ndefu kukabili mabadiliko ya tabianchi hivyo..(Sauti ya Balozi Louise)

“Hatupaswi kusalia kuridhika na utiwaji saini pekee siku ya leo. Kazi yenyewe inaanza sasa ya kuridhia mkataba na kufananisha ahadi zetu na vitendo.”

Kwa mantiki hiyo amesema serikali ya Rwanda kwa upande wake itachukua hatua zote muhimu ili kuridhia mkataba huo haraka iwezekanavyo na iko tayari kutekeleza wajibu wake.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter