Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Ufaransa afurahia hatua ya kihistoria kwa ajili ya tabianchi

Rais wa Ufaransa afurahia hatua ya kihistoria kwa ajili ya tabianchi

Nchi zilizoendelea zinapaswa kuonyesha mfano katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia nchi zinazoendelea kwenye jitihada hizo, amesema leo Rais wa Ufaransa Francois Hollande kwenye hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi inaofanyika leo mjini New York Marekani.

Kwenye hotuba yake Rais Hollande amekumbusha kwamba makubaliano yaliyoafikiwa mjini Paris mwezi Disemba mwaka uliopita yalikuwa ya kihistoria na yameonyesha kwamba nchi zote zinaweza kulegeza misimamo yao na kushikamana kwa ajili ya sayari ya dunia.

Amesisitiza kwamba ni lazima kuongeza bidii ili ahadi zilizotolewa zigeuke hatua, wakati ambapo uharibifu wa mazingira unaendelea kwa kasi kubwa. Hatua inayofuata, amezingatia, ni mabunge kuridhia mkataba huo, akihimiza jitihada zifanyike ili angalau nchi 55 zinazowakilisha asilimia 55 ya utoaji wa gesi chafuzi duniani kote ziridhie mkataba huo.

Amesisitiza umuhimu wa kuweka bei kwa hewa ya mkaa.

(Sauti ya Rais Hollande)

“Natoa ahadi kwa niaba ya Ufaransa, ili, haraka iwekezanavyo, bei ya hewa ya mkaa ibainiwe, kwanza, Ufaransa, Ulaya halafu duniani kote, ni msingi ili tuweza kukuza uchumi mpya.”