Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni wakati wa kugeuza ahadi kuwa hatua madhubuti- Kabila

Sasa ni wakati wa kugeuza ahadi kuwa hatua madhubuti- Kabila

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila, amesema leo ni fursa ya kuweka ratiba ya kuhakikisha Mkataba wa Paris utakuwa na mamlaka kamili katika sheria ya kimataifa, na kwamba utatekelezwa. Taarifa kamili na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Akizungumza kwa niaba ya nchi yake na nchi 48 zinazoendelea, Rais Joseph Kabila amesema maazimio ya leo ya hatua kabambe kutoka kwa viongozi wa dunia, yanatoa ishara thabiti kuwa wakati umewadia wa kugeuza matarajio kuwa hatua madhubuti.

“Kwa mantiki hiyo, mawaziri kutoka nchi zinazoendelea walikutana mjini Kinshasa mapema mwezi huu kukariri dhamira zao kuhusu Mkataba wa Paris. Walisema kuwa serikali zao zitachukua hatua zote zinazohitajika kuuridhia Mkataba wa Paris haraka iwezekanavyo.”

Rais Kabila amesema Mkataba wa Paris unaweka changamoto nyingi na fursa kwa uchumi wa nchi masikini, na kwamba ili kufikia malengo mengi yaliyowekwa katika Mkataba huo kwa uhakika na kwa kiwango kikubwa, fedha zaidi na rasilmali nyinginezo ni lazima ziwekezwe.