Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa Paris lazima utoe afueni ya muda mrefu ya mabadiliko ya tabia nchi:UNISDR

Mkataba wa Paris lazima utoe afueni ya muda mrefu ya mabadiliko ya tabia nchi:UNISDR

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya upunguzaji hatari ya majanga UNISDR, Robert Glasser, leo ametoa wito kwa watakaotia saini mkataba wa Paris kwenda mbali zaidi ya majukumu yao yaliyopo ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kama wanataka dunia kuepuka zahma kubwa za hali ya hewa siku za usoni.

Bwana, Glasser amekaribisha hatua ya nchi 160 kutangaza watatia saini mkataba huo, lakini akaonya kwamba dunia iko hatarini kughubikwa na kasi kubwa ya ongezeko la joto endapo watia saini hao hawataongeza juhudi zao katika kupunguza gesi chafu.

Amesema ni dhahiri kwamba hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi vinahusishwa kwa asilimia 90 na majanga makubwa ya asili.

Ukame, mafuriko, vimbunga na joto la kupindikia vina uwezekano mkubwa wa kuathiri juhudi za nchi zinazoendelea za kutokomeza umasikini.