Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA atoa wito wa msaada kwa waathirika wa tetemeko Ecuador

Mkuu wa OCHA atoa wito wa msaada kwa waathirika wa tetemeko Ecuador

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA , Bwana Stephen O’Brien leo amehitimisha ziara ya siku mbili nchi Ecuador na kutoa wito wa misaada aidi kwa watu walioathirika na tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo Jumamosi iliyopita.

Amesema maelfu ya watu wamepoteza ndugu zao, nyumba zao na maisha yao, lakini ametiwa moyo na ujasiri walionao , na kwamba hatua zilizochukuliwa na serikali ya Ecuador na jamii kwa ujumla zimeokoa maisha ya watu wengi.

Mamia ya watu wameuawa kwenye tetemeko hilo, maelfu kujeruhiwa na zaidi ya watu 720,000 wameathirika kwaa njia moja au nyingine. Hivi sasa serikali, wahudumu wa dharura, chama cha msalaba mwekundu na mashirika mengine wanashirikiana kuwapa watu msaada wa chakula, maji ya kunywa, malazi, msaada wa matibabu na huduma nyingine za msingi ikiwa ni pamoja na kurewjesha huduma ya umeme.

Akiwa Ecuador bwana O’Brien amezuru miji ya Manta, Canoa, Jama, Pedernales na Portoviejo na kukutana na watu waliopoteza kila kitu.