Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa yaongeze juhudi kufikia lengo la nyuzi joto 1.5 °C:UM

Mataifa yaongeze juhudi kufikia lengo la nyuzi joto 1.5 °C:UM

Utiaji saini wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi hapo Ijumaa April 22, ni hatua ya kihistoria kuelekea katika hakikisho kwamba vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi vinazingatia athari kwa haki za binadamu.

Hayo ni kwa mujibu wa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira John Knox. Ameyataka mataifa kutumia fursa hii kuonyesha uwajibikaji wao katika kuhakikisha ongezeko la joto duniani linasalia kuwa chini ya nyuzi joto 2.

Amesema mkataba wa Paris ni mafanikio makubwa kwa dunia, kwa sababu unatambua kwamba kuheshimu haki za binadamu ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza mkataba wa kimataifa wa mazingira umetaja bayana haki za binadamu.

Mkataba wa Paris ulipitishwa Desemba 12 mwaka 2015 na unatoa wito kwa pande zote kuheshimu na kuchagiza haki za binadamu zinapochukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.