Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walokumbwa na mapigano Benghazi wahamishwe kwa usalama:Kobler

Walokumbwa na mapigano Benghazi wahamishwe kwa usalama:Kobler

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL, Martin Kobler, ametoa wito kwa pande zote hasimu zinazopigana mjini Benghazi kuhakikisha kwamba raia wanalindwa.

Amezitaka pande zote kuruhusu na kusaidia watu waliokwama katika maeneo ya mapigano ambao wanataka kuondoka, waondoke kwa usalama mara moja.

Bwana Kobler amesema raia wote, wanawake, wanaume au watoto, wawe raia wa Libya au wageni wanaotaka kuondoka maeneo ya Benghazi ni lazima waruhusiwe kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

Pande kinzani ni lazima zihakikishe raia wako huru kuondoka na kwa usalama, pia amesema waliojeruhiwa wapatiwe huduma na kila mmoja atendewe ubinadamu kwa misingi ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Kobler amezikumbusha pande zote kinzani wajibu wao wa kuheshimu sharia za kimataifa na haki za binadamu na wale watakaoshindwa kufanya hivyo lazima wawajibishwe.