Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya kitaifa dhidi ya Polio Yemen yakamilika

Kampeni ya kitaifa dhidi ya Polio Yemen yakamilika

Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na wizara ya afya ya Yemen wamehitimisha kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya Polio nchini humo iliyolenga watoto zaidi ya Laki Tano wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba ilijumuisha wafanyakazi Elfu 40 wa afya ambapo wawakilishi wa mabaraza ya mitaa na mashirika ya kiraia walishiriki kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.

Dkt. Ahmed Shadoul, mwakilishi wa shirika la afya duniani, WHO nchini Yemen amesema kampeni ilifikia hadi watoto kwenye maeneo magumu kufikika ikiwemo wakimbizi hata wale wa ndani.

Polio ilikuwa imetokomezwa Yemen hadi mwaka 2006 na WHO na shirika la kuhudumia watoto UNICEF yanahakikisha mzozo unaoendelea hautafuta mafanikio yaliyopatikana na kurejesha ugonjwa huo hatari.