Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Historia kuandikwa April 22, dunia ikitia saini mkataba wa COP21

Historia kuandikwa April 22, dunia ikitia saini mkataba wa COP21

Hayawai hayawi sasa yatakuwa, Ijumaa historia kuandikwa Ijumaa April 22, wakati viongozi wa dunia wakikusanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York kutia saini mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi walioupitisha Disemba mwaka 2015 ujulikanao COP21. Lakini safari ya kufikia ukurasa huu wa kihistoria imekuaje? Flora Nducha anatanabaisha

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mikutano na mikutano imefanyika karibu kila kona ya dunia,katika safari ya kupambana na mabadiliko ya tabia mchi kuanzia mwaka 1992 ulipofanyika mkutano wa Rio ‘earth summit” na kwa miaka zaidi ya 20 kumekuwa na mikataba kadhaa kabla ya kuafikiwa mkutano mkuu wa COP21 uliofanyika Paris Disemba mwaka 2015, lengo likiwa kuwa la kauli moja ya kimataifa ambayo itaibana dunia kisheria katika kupunguza kiwango cha joto duniani na kufikia nyuzi joto chini ya 2.

Debe likapigwa na shime ikatiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumzwa kwenye mkutano COP21
(SAUTI YA BAN COP 21)

“Maamuzi yatakayochukuliwa Paris yatajenga muskhbali wa dunia yetu, na jamii ya binadamu kwa karne zijazo, na ndio maana tunahitaji mkataba kabambe, na lazima tukabiliane na changamoto za mabadiliko ya tabia nnchi. Nnawaomba nyie raia wa dunia, wafahamisheni viongozi wenu , wajue kwamba wakati umewadia wa mkatana wenye nguvu unaokwenda sanjari na vitendo”

Ujumbe ukafika na wito ukaitikiwa na hapo Novemba 30 hadi Desemba 12 viongozi wa dunia, makampuni, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, watu mashuhuria na wadai mbalimbali wa kupigia upatu mabadiliko ya tabia nchi wakakusanyika Paris Ufaransa kuandika historia kwa kauli moja. Wakapitisha mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi ambao Karen Christiana Figueres katibu mkuu wa mkakati wa Umoja wa mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi (UNFCCC) alikuwa akiuota kila uchao.

image
Christiana Figueres, katibu Mkuu wa UNFCCC.(Picha:UNFCCC/flickr)
(SAUTI YA CHRISTIA FIGUERES)

“Nimekuwa nikisema kwa muda mrefu, ni lazima tufanye, tunaweza, na nimikuwa nikisema tutafanya, leo tunaweza kusema tumefanya na nawashukutu wote”

Nderemo na vificho vikatawala na hii ni baada ya nchi 195 kuridhia mkataba huo naye Rais wa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius akatangaza rasmi kupitishwa kwa mkataba huo.

image
Rais wa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius.(Picha:UM/Mark Garten)
(SAUTI YA FABIUS)

"Naangalia ukumbi, naona watu wamefurahia nasioni anayepinga, hivyo mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi umepitishwa.”

Na baada ya ngwe hiyo sasa macho na masikio yote yanaelekezwa hapa New York makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Ijumaa tarehe 22 Aprili ukurasa mpya wa kihistoria utafunuliwa na wawakilishi wa mataifa 160 wanatarajiwa kushika kalamu na kutia saini mkataba huo wa Paris ili uanze utekelezaji.

Miongoni mwao ni wakuu wa nchi 60 wakiwemo Rais wa Ufaransa François Hollande, makamu waziri mkuu wa Uchina Zhang Gaoli, waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Usikose kujiunga nasi kwa habari na matukio kemkem kwenye tovuti yetu na pia moja kwa moja kwenye Facebook.