Ukwepaji sheria Maziwa Makuu watafutiwa mwarubaini Nairobi

Ukwepaji sheria Maziwa Makuu watafutiwa mwarubaini Nairobi

Waendesha Mashtaka kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika, wamekutana jijini Nairobi kwa minajili ya kuafikia njia mwafaka na fanisi za ushirikiano wa kikanda katika kupambana ukwepaji sheria.

Mkutano huo wa Aprili 19 na 20, uliandaliwa na Kongamano la Kimataifa kuhusu Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), kwa ushirikiano na Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu.

Mkutano huo wa siku mbili ulilenga kuboresha uelewa wa changamoto na vizuizi dhidi ya ushirikiano katika masuala ya kisheria ukanda wa Maziwa Makuu, kuvumbua fursa za kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha ushirikiano huo, na kuridhia njia mwafaka ya ushirikiano wa kisheria unaojumuisha utekelezaji wa sheria za kitaifa zinazotokana na mikataba ya ICGLR kuhusu ushirikiano kama huo.

Mkutano huo unafuatia ule wa Mawaziri wa Sheria uliofanyika mjini Livingstone, Zambia, kati ya Agosti 25 na 26 mwaka 2015.