Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa Bahari ya Mediterenia wasimulia yaliyowasibu

Manusura wa Bahari ya Mediterenia wasimulia yaliyowasibu

Manusura wa moja ya mikasa mikubwa zaidi baharini katika mwaka mmoja uliopita wameanza kusimulia kilichowasibu, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Ni watu 41 tu ndio waliookolewa na meli ya biashara, baada ya boti lao kuzama katika Bahari ya Mediterenia wiki iliyopita na kuwaua watu wanaokisiwa kuwa 500.

Kulingana na UNHCR, manusura hao ni sehemu ya kundi la watu wengine kati ya 100 na 200 walioondoka pwani ya Libya karibu na mji wa Torbuk, wakielekea Italia.

Wakiwa safarini baada ya saa kadhaa baharini, wasafirishaji haramu wa watu waliwalazimisha kupanda boti lingine kubwa ambalo tayari lilikuwa na mamia ya watu, na ni wakati huo wa kuwahamisha ndipo boti hilo lilipinduka na kuzama.

William Spindler ni msemaji wa UNHCR, Geneva

“Manusura bila shaka wameshtushwa sana na walichokiona. Wengine wao waliona jamaa zao wakifariki dunia. Wamepitia masahibu mabaya sana”

Manusura hao, ambao ni wanaume 37, wanawake watatu na mtoto mmoja mwenye umri wa miaka mitatu, walielea baharini kwa siku tatu kabla ya kuokolewa na kupelekwa Kalamata, Ugiriki.