Uganda inajitahidi kupambana na dawa za kulevya, lakini kuna changamoto

Uganda inajitahidi kupambana na dawa za kulevya, lakini kuna changamoto

Uganda imepiga hatua katika kudhibiti dawa za kulevya na fursa ya matibabu kwa waathirika amesema mwakilishi wa kudumu wa Uganda kwenye Umoja wa mataifa Dr Richard Nduhuura.

Akizungumza kwenye kongamano maalumu kuhusu matatizo ya dawa za kulevya duniani linalokamilika kesho Alhamisi hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa Nduhuura ameongeza kuwa miongoni mwa hatua Uganda ilizochukua moja ni kupitia upya sheria ya kuimarisha hatua za kudhibiti matumizi na usafirishaji haramu wa dawa hizo pamoja na kifungo kwa mujibu wa viwango na sheria za kimataifa.

Pili ni kufanyia mabadiliko sheria ili kuruhusu mafunzo muafaka kwa wauguzi na maafisa wa afya kuweza kuwaandikia wagonjwa baadhi ya dawa ambazo ni kali kwa ajili ya maumivu.

Hata hivyo amesema pamoja na hatua hizo kuna changamoto kama vile matumizi ya opiods kwa ajili ya matibabu na kisayansi bado ni madogo kwa viwango vya Afrika na kimataifa, pia ushirikiano mdogo miongoni mwa vitengo vinavyohusika na udhibiti wa dawa za kulevya, pia uwezo mdogo wa kifedha, teknolojia na nguvu kazi mipakani ili kushughulikia ongezeko la usafirishaji haramu wa dawa hizo kupitia Uganda.