Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban afuatilia mchakato wa kesi dhidi ya NGOs huko Misri

Ban afuatilia mchakato wa kesi dhidi ya NGOs huko Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anafuatilia kwa karibu kesi inayoendelea hii leo huko nchini Misri dhidi ya mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za binadamu.

Ban amesema katika kesi hiyo namba 173 inayotambuliwa kama kesi kuhusu mashirika ya kiraia kupokea michango ya fedha kutoka nje ya nchi, washtakiwa wanapaswa kupata haki yao ya msingi ikiwemo kesi kuendeshwa kwa haki.

Amesisitiza umuhimu wa mashirika ya kiraia katika kuhakikisha serikali zinawajibika kwa raia wake akiongeza kuwa ni vyema watetezi wa haki za binadamu na mashirika hayo kwa ujumla na vyombo vya habari kufanya kazi bila vizingiti visivyo na msingi.

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa serikali ya Misri kupitia mfumo wa kila mwaka wa tathmini wa utendaji wake wa haki za binadamu ilikubali mapendekezo kadhaa ikiwemo kulinda na kutetea uhuru wa kujiunga na vikundi na kuridhia sheria mpya ya mashirika ya kiraia inayoendana na haki za binadamu za kimataifa.