Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wawili wafariki dunia kwenye maandamano Mali- MINUSMA

Watu wawili wafariki dunia kwenye maandamano Mali- MINUSMA

Watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, na wengine wanne kujeruhiwa kwenye vurugu nchini Mali, wakati wa maandamano makali yaliyofanyika siku ya Jumatatu mjini Kidal.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA, umesema kwamba katika maandamano hayo yaliyofanyika kwenye eneo la uwanja wa ndege, waandamanaji walirusha mabomu ya petroli na kuteketeza miundombinu ya uwanja wa ndege.

MINUSMA imepeleka salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia nafuu waliojeruhiwa.

Aidha MINUSMA imeeleza kwamba imeshaunda tume ya uchunguzi ambayo imeanza kazi yake ya kubuni ukweli kuhusu asili ya risasi zilizofiatuliwa, ikisema iko tayari kuchukua hatua za kisheria, iwapo itahitajika.

Uwanja huo wa ndege ulikuwa ukilindwa na MINUSMA, ambayo ilihitimisha ukarabati wa eneo hilo miezi michache iliyopita.

Ikikariri wito wa utulivu kwa ushirikiano na mamlaka za serikali ya Mali na viongozi wa jamii, MINUSMA imesisitiza kwamba uwanja wa ndege ni sehemu muhimu kwa kufikisha misaada ya kibinadamu pamoja na kupeleka vifaa kwa ajili ya walinda amani.