Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malori ya WFP yapeleka msaada wa chakula Ecuador

Malori ya WFP yapeleka msaada wa chakula Ecuador

Shirika la Mpango wa Chakula, WFP, limepeleka msaada wa chakula kwa watu wapatao 8,000 walioathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi pwani ya Ecuador.

Tetemeko hilo liliwaua zaidi ya watu 400 na kuwaacha maelfu ya wengine wakihitaji usaidizi wa kibinadamu kwa dharura.

Kwa ombi la serikali ya Ecuador, WFP na mamlaka za nchi hiyo zimeandaa malori yaliyosheheni chakula cha kutosha kulisha watu 8,000 kwa kipindi cha siku 15 katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Aidha, msaada wa ziada wa chakula utapelekewa watu wengine 12,000 na wagonjwa 1,000 hospitalini walioathiriwa na tetemeko hilo la ardhi.

Taarifa ya WFP imesema shirika hilo limeandaa timu za dharura kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika ili kutathmini hali ya kibinadamu na uhakika wa kupata chakula.