Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kusaidia Haiti kukabiliana na ukame

WFP kusaidia Haiti kukabiliana na ukame

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP), linatarajia kuzindua operesheni ya dharura ya kusaidia watu wapatao milioni 1 walioathirika na ukame nchini Haiti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WFP, watu takriban milioni 3.6, sawa na theluthi moja na idadi ya watu wote nchini Haiti, wanakabiliwa na ukosefu wa chakula kutokana na ukame uliodumu kwa miaka mitatu na ulioongezeka kwa sababu ya El-Nino.

Mkurugenzi Mkuu wa WFP Ertharin Cousin amenukuliwa akisema ni lazima kusaidia raia wa Haiti, na kuhakikisha hakuna mtoto anayeshinda na njaa kwa sababu ya umaskini wala ukame.

Amesema hayo alipohitimisha ziara yake ya siku tatu nchini Haiti ambapo amekutana na jamii zilizoathirika na ukame.

Kwa mujibu wa tathmini ya WFP, ukame na ukosefu wa pembejeo za kilimo, umesababisha upungufu wa asilimia 82 ya mavuno na mfumko wa bei za vyakula wa asilimia 60.