Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waridhishwa na kuachiliwa kwa wafungwa Myanmar

Umoja wa Mataifa waridhishwa na kuachiliwa kwa wafungwa Myanmar

Kamishna Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Zeid Ra'ad al Hussein, amekaribisha leo kuachiliwa huru kwa wafungwa 83 nchini Myanmar ambao miongoni mwao ni wanaharakati wa haki na waandishi wa habari.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu imeeleza kwamba wafungwa hao wamesamehewa na Rais mpya wa Myanmar, U Htin Kyaw. Uamuzi huo unafuatia uamuzi mwingine uliochukuliwa awali mwezi Aprili ambapo wafungwa 199 waliokamatwa kwa misingi ya kisiasa wameachiliwa huru pia, wakiwemo wanafunzi.

Kwa mujibu wa serikali ya Myanmar, hatua hizo zinalenga kukuza maridhiano ya kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi leo, msemaji wa Ofisi ya Haki za binadamu, Ravina Shamdasani, amesema hatua hizo ni ishara ya mwelekeo mzuri katika kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa zaidi nchini Myanmar.

Bi Shamdasani amesema Ofisi yake inaishauri serikali ya Myanmar kuachilia huru wafungwa wengine waliofungwa kwa misingi ya kisiasa na kidini.