Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapongeza Jordan kuruhusu wakimbizi wa Syria kufanya kazi

UNHCR yapongeza Jordan kuruhusu wakimbizi wa Syria kufanya kazi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limekaribisha hatua mfululizo za serikali ya Jordan zinazowezesha wakimbizi wa Syria kupata kazi kihalali nchini humo.

Ikikaribisha hatua hiyo, UNHCR imenukuliwa ikisema kuwa hatua hiyo itawasaidia wakimbizi wajitegemee ambapo inakadiriwa kuwa takribani wakimbizi 78,000 watapata kazi ndani ya kipindi kifupi na maelfu wakitarajiwa kuneemeka siku za usoni.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Jordan katika siku za hivi karibuni ni mpango wa siku 90 unaowaruhusu waajiri katika sekta zisizo rasimi kupata bure vibali vya kufanyia kazi kwa ajili ya wakimbizi wa Syria.

Mpango huo unawawezesha wakimbizi hao kufanya kazi kama wahamiaji wengine, kazi zikiwa mathalani za ujenzi, kilimo, viwandani, vyakula na vinywaji pamoja na maeneo ya mauzo ya jumla.