Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mmiminiko wa wakimbizi wa Sudan Kusini waendelea, UNHCR yaripotia uhaba wa fedha

Mmiminiko wa wakimbizi wa Sudan Kusini waendelea, UNHCR yaripotia uhaba wa fedha

Nchini Sudan Kusini, hali ya raia inaripotiwa kuzidi kuzorota kutokana na mapigano mapya, kutokuwepo uhakika wa kupata chakula katika majimbo ya Bahr El Ghazal na Warrap, pamoja na uhaba wa ufadhili, limesema Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Kwa mujibu wa UNHCR, mapigano ya hivi karibuni kati ya vikosi vya serikali na upinzani Magharibi mwa Bahr El Ghazal, yamesababisha zaidi ya watu 96,000 kukimbilia mji wa Wau, kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini.

Ariane Rummery ni msemaji wa UNCHR, Geneva..

“Takriban raia 52,000 wa Sudan Kusini wamekimbilia Sudan tangu mwishoni mwa Januari. Uganda pia imeshuhudia ongezeko kubwa la wakimbizi wanaowasili, wakati mwingine hadi watu 800 kwa siku. Nchi zingine ni Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Kenya. Watu milioni 2.3 wamekimbia makwao tangu machafuko yalipoanza Sudan Kusini mnamo Disemba 2013.”

Nchi zote jirani sasa zinaripoti ongezeko katika mmiminiko wa wakimbizi, huku mpango wa kikanda wa kuwasaidia wakimbizi ukiwa umepata asilimia nane tu ya ufadhili unaohitajika, na huduma za kunusuru maisha zikiwa mashakani.