Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kingono bado huathiri jamii Mali: Zainab Bangura

Ukatili wa kingono bado huathiri jamii Mali: Zainab Bangura

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ukatili wa kingono vitani, Zainab Hawa Bangura, amehitimisha ziara yake nchini Mali, akisisitiza harakati zinazopaswa kuchukuliwa ili kuimarisha usalama, utawala wa sheria na huduma za kijamii nchini humo.

Bi Bangura amesema, licha ya kutiwa matumaini na makubaliano ya amani, bado wanawake wako hatarini kukumbwa na ukatili wa kingono na manusura wanaendelea kuathirika.

Kwenye taarifa iliyotolewa jumapili hii, Bi Bangura amenukuliwa akilaani jinsi vikundi vya kigaidi vinavyotumia kisingizio cha dini ya kiislamu kushawishi vijana na kuwaruhusu kuteka nyara wanawake au kuwabaka. Amesema ni vitendo hivyo ni kutoheshimu dini kabisa.

Katika ziara yake amezungumza na Waziri Mkuu Modibo Keita, viongozi wengine wa kisiasa, kijamii na kidini, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya wanawake na hata wawakilishi wa waasi. Amepata fursa pia ya kuzungumza na manusura ya ukatili wa kingono mjini Timbuktu kaskazini mwa nchi.