Skip to main content

Ban Ki-moon ataka juhudi mpya katika mchakato wa amani wa Israel na Palestina

Ban Ki-moon ataka juhudi mpya katika mchakato wa amani wa Israel na Palestina

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati, Katibu Mkuu Ban Ki-moon akiwaeleza wanachama kwamba jitihada za kimataifa zinakumbwa na vitendo vya Israel na Palestina vinavyoharibu mchakato wa amani na kuhatarisha uwezekano wa kuwepo kwa suluhu ya mataifa mawili.

Kwenye hotuba yake, Bwana Ban ametaja harakati za serikali ya Israel za kubomoa nyumba za wapalestina na vile vile kuenea makazi ya walowezi, pia mashambulizi ya kigaidi ya baadhi ya wapalestina dhidi ya Israel na mivutano ya kisiasa baina ya vyama vya Palestina.

Katibu Mkuu ameeleza kusikitishwa sana na vurugu inayoongezeka baina ya Israel na Palestina kwa zaidi ya miezi sita iliyopita, ambapo waisrael 30 na wapalestina 200 wameuawa.

Aidha amesikitishwa kwamba zaidi ya mwaka mmoja na nusu baada ya mzozo ulioathiri mji wa Gaza, bado ukarabati wa miundumbinu haujatimizwa.

(Sauti ya Ban)

“Njia ya kutatua mkwamo wa kisiasa ni kujituma, kulegeza misimamo, kuheshimiana na kuonyesha uongozi kutoka pande zote mbili. Pia ni lazima, kupitia vitendo pamoja na maneno – kukariri msimamo kwamba suluhu ya mataifa mawili ndio suluhu ya pekee inayoweza kuridhisha matarajio ya raia wote. Israel, na Palestina, zikiishi pamoja kwa amani, kutambuana panse zote”.

Halikadhalika, amezungumzia mahitaji ya nchi zilizopakana na Syria, ambazo hukumbwa na changamoto kubwa kutokana na wimbi la wakimbizi, huku akipongeza ahadi za nchi nane na Muungano wa Ulaya za kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.