Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea UNGASS, haki za binadamu zipewe kipaumbele: Wataalamu

Kuelekea UNGASS, haki za binadamu zipewe kipaumbele: Wataalamu

Kuelekea kikao maalum cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu tatizo la dawa za kulevya duniani UNGASS, kinachoanza kesho, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wamezitaka nchi wanachama kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa katika kudhibiti dawa hizo.

Katika tamko lao wataalamu hao wamesema wanaamini UNGASS inatoa fursa muhimu katika kutathimini mafanikio na changamoto katika kudhibiti dawa kimataifa na madhara yake katika kutimiza haki za binadamu na haki za kimsingi.

Taarifa hiyo imewananukuu wataalamu hao wa haki za binadamu wakisema kuwa uchunguzi wao kuhusu madhara ya haki za binadamu katika udhibiti wa kimatiafa wa dawa za kulevya, unaonyesha wasiwasi mkubwa kutokana na sera zinaoongeza hatari ya uvunjifu wa haki za binadamu.

Wamesema wana wasiwasi kwamba mfumo wa sasa wa kimataifa wa kudhibiti dawa za kulevya unatoa adhabu kupita kiasi, sera nyingi za kitaifa zina misingi ya kibaguzi, za kufungwa jela na utekelezaji wa sheria umekuwa kikwazo katika ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu.