Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo ni msingi wa kupata amani ya kudumu CAR- FAO

Kilimo ni msingi wa kupata amani ya kudumu CAR- FAO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva leo amekuwa na mazungumzo na Rais Faustin-Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR huko Roma, Italia wakijikita katika jinsi ya kujenga upya sekta ya kilimo nchini humo kama kichochea cha amani na maendeleo endelevu.

Mathalani wamejadili jinsi ya kutumia vyema fursa nzuri ya mazingira bora ya kilimo CAR na kusaidia familia zinazohusika na kilimo, wakulima wadogo ili kuimarisha uhakika wa chakula, lishe na kuinua kipato cha kaya.

Yaelezwa kuwa Rais Touadera ambaye alishinda uchaguzi mwezi uliopita amepatia kipaumbele kilimo na uchumi wa vijijini ili kusongesha nchi yake ambako asilimia 75 ya wananchi wanategemea sekta ya kilimo.

(Sauti ya Rais Touadera)

“Tunaanza hivi karibuni utaratibu wa kujisalimisha kwa waasi, na FAO inataka kusaidia pia katika eneo hilo kwa kusaidia vijana ambao watarejea kwenye jamii baada ya kujisalimisha. Watapata msaada kwenye vijiji vyao ikiwemo kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi.”