Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon ahimiza uwekezaji na usaidizi wa kimataifa

Ban Ki-moon ahimiza uwekezaji na usaidizi wa kimataifa

Nchi maskini zaidi duniani zinaathirika zaidi na hatari za majanga, njaa, na mizozo lakini vile vile zina fursa kubwa zaidi za maendeleo amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipohudhuria mkutano wa mawaziri wa nchi maskini zaidi duniani, mjini Washington, Marekani.

Mkutano huo umefanyika sanjari ya mkutano wa Shirika la Fedha duniani IMF na benki ya dunia ambao maudhui yake mwaka huu ni mzozo wa wakimbizi.

Bwana Ban amesisitiza umuhimu kwa nchi hizo maskini kupaza sauti zao katika mikutano ya kimataifa.

Halikadhalika, Katibu Mkuu amehutubia kongamano lililofanyika mjini Washington siku hiyo ya jumamosi kuhusu miundumbinu akizingatia umuhimu wa uwekezaji katika huduma za maji safi na usafi na umeme.

Bwana Ban amesema msaada wa jamii ya kimataifa unaweza kupunguza tofauti baina ya nchi katika upatikanaji wa huduma hizo, kwa kuheshimu ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.