Ban Ki-moon atoa wito wa mshikamano wa kimataifa kwa wakimbizi

Ban Ki-moon atoa wito wa mshikamano wa kimataifa kwa wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mshikamano wa kimataifa unahitajika ili kukabiliana na mzozo wa wakimbizi unaoikumba dunia ya leo.

Katibu Mkuu amesema hayo akihutubia mkutano wa kimataifa kuhusu watu wanaolazimika kuhama makwao ulioandaliwa na Shirika la Fedha duniani IMF na Benki ya Dunia mjini Washington, Marekani.

Akieleza jinsi mwenyewe alivyopitia wakati mgumu wa ukimbizi wa ndani akiwa mtoto na alivyosaidiwa na Umoja wa Mataifa nchini Korea, Bwana Ban amesitiza kwamba viongozi wanapaswa kuwapatia wakimbizi na wahamiaji makazi na njia halali za hifadhi.

Ameongeza kwamba kupokea wakimbizi kunaweza kuwa faida kwa nchi kwani wanaleta utalaam wao, utashi wa kujifunza na kufanya kazi wakati ambapo wafanyakazi wengi hasa Ulaya wameshazeeka.

(Sauti ya Bwana Ban)

“Kuwaharamisha siyo tu vibaya kimaadili, pia siyo sahihi. Tunapaswa kutambua kwamba mzozo wa wakimbizi na wakimbizi wa ndani ni ishara ya changamoto kubwa zaidi. Nchi nyingi mno, hata ukanda mzima, zinakumbwa na mzunguko wa vurugu, ghasia na umaskini.”

Amesema suluhu ni kukabiliana na sababu za msingi na mizizi ya mizozo zikiwa ni ukosefu wa usalama, utawala duni na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.

Kwa mujibu wa UNHCR, watu milioni 60 duniani kote ni wakimbizi, wakimbizi wa ndani au wasaka hifadhi, nusu yao wakiwa ni watoto.