Mtazamo mpya kukabili hali ya HIV kwa wanaojichoma dawa za kulevya unahitajika:UNAIDS

Mtazamo mpya kukabili hali ya HIV kwa wanaojichoma dawa za kulevya unahitajika:UNAIDS

Kabla ya kuanza kwa kikao maalumu cha baraza kuu la Umoja wa mataifa kuhusu tatizo la mihadarati duniani , shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na vita dhidi ya ukimwi UNAIDS limetoa ripoti mpya iitwayo “Usidhuru:afya, haki za binadamu na watu wanaotumia dawa za kulevya”. John Kibego na taarifa kamili.

(TAARIFA YA KIBEGO)

Kwa mujibu wa UNAIDS, ripoti hiyo inaonyesha kwamba kushindwa kwa nchi nyingi kuchukua mtazamo wa afya na haki za binadamu kumesababisha kutopungua kimataifa idadi ya visa vipya vya maambukizi ya HIV miongoni mwa watu wanaojidunga dawa za kulevya kati ya mwaka 2010 na 2014.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibé, amesema suala la kuchukulia maisha kama kawaida, halijaifikisha dunia popote na ni lazima ijifunze kutokana na miaka 15 iliyopita na kufuata mfano wan chi ambazo zimeweza kubadili hali ya maambukizi miongoni mwa wanaotumia dawa za kulevya kwa kuchukua mtazamo wa kupunguza madhara kwa kutoa kipaumbele kwa afya na haki za binadamu.Kama anavyofafanua msemaji wa UNAIDS Monique Middelhoff

(SAUTI YA MONIQUE MIDDELHOFF)

“Tunachokishuhudia ni kwamba mtazamo wa upunguzaji madhara tayari ni wa kimataifa, unatekelezwa Kazakhstan, Malaysia, Uchina,Ulaya , na afrika nchi kama Tanzania na Kenya, hivyo inawezekana.”

Kikao maalumu cha baraza kuu kuhusu tatizo la dawa za kulevya duniani kitafanyika April 19 hadi 21 hapa New York.