Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lahitimisha kusikiliza wanaowania wadhifa wa Ban Ki-moon

Baraza Kuu lahitimisha kusikiliza wanaowania wadhifa wa Ban Ki-moon

Ni rais wa Baraza Kuu, Morgens Lykketoft, akifungua vikao vya leo vya Baraza Kuu, katika mchakato wa kihistoria ulio wazi na jumuishi, wa uteuzi wa Katibu Mkuu mpya atakayemrithi Ban Ki-moon, ambaye anahitimisha muhula wake mwishoni mwa mwaka huu. Maneno yake ni yale yale aliyotumia katika vikao vya vya awali Jumanne na Jumatano, akisisitiza utoaji fursa na muda sawa kwa wagombea na wajumbe wa nchi wanachama wanaouliza maswali.

image
Picha kapsheni: Vuk Jeremić, raia wa Serbia na Rais wa Kikao cha 67 cha Baraza Kuu la UM. Picha:UM/ Webcast.
Wa kwanza kuzungumza katika kikao cha asubuhi, alikuwa ni Vuk Jeremić, raia wa Serbia, ambaye alikuwa rais wa kikao cha 67 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambaye amesema wakati huu ni muhimu sana kwa kizazi cha sasa, akitaja misingi mitatu inayohitajika kuifanikisha kazi ya Umoja wa Mataifa

“Mosi, kuhakikisha kuwa uamuzi wa pamoja unawakilisha mtandano imara zaidi wa usalama katika changamoto za sasa. Pili, kwamba Umoja wa Mataifa uliofanyiwa marekebisho unapaswa kuwa kiungo cha kati cha utawala wa kimataifa. Na tatu, kwamba rasilmali zilizopo za Umoja wa Mataifa zinatumiwa vyema zaidi, ili uweze kupata ufanisi wanaotaka wanachama wake na jamii ya kimataifa kwa ujumla.”

image
Picha kapsheni: Helen Clark, Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand na Mkuu wa UNDP, akiwa mmoja wa wagombea wa wadhfa wa Katibu Mkuu Picha ya UM/Rick Bajornas.
Wa pili katika vikao vya leo amekuwa ni Bi. Helen Clark, Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand na Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP). Bi Clark ambaye pia ni mmoja wa wanawake wanne wanaogombea wadhfa wa Katibu Mkuu, amesema miaka 70 tangu kuasisiwa kwake, Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto kubwa, ambazo ni mtihani kwa uwezo wake kupata ufanisi

“Lakini tunapaswa kujitahidi zaidi, kupitia kushirikiana kwa karibu zaidi, mazungumzo, na kujenga ubia mpana tunavyoweza. Nadhani Umoja wa Mataifa unaweza kupata ufanisi zaidi katika kuhudumia nchi wanachama, na unaweza kuwa mahali bora zaidi pa kufanya kazi. Ni lazima uwe wazi kuhusu unachoweza kufanya na usichoweza kufanya. Ni lazima ushirikiane na nchi wanachama kuona kuwa rasilmali unazopewa zinaelekezwa zaidi panapoweza kupatikana mabadiliko makubwa zaidi”

image
Picha kapsheni: Dkt. Srgjan Kerim wa Macedonia, Rais wa kikao cha 62 cha Baraza Kuu na mmoja wa wagombea wadhfa wa Katibu Mkuu Picha: UM/Rick Bajornas
Na wa mwisho katika vikao vya leo amekuwa ni Dr. Srgjan SHRIJYAN  Kerim, raia wa Macedonia, ambaye alikuwa rais wa kikao cha 62 cha Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa. Akiwasilisha hoja na mtazamo wake, Dr. Kerim amesema ajenda yake inatokana na masuala yanayopewa kipaumbele na Umoja wa Mataifa na kilichowekwa na nchi wanachama

“Inatoa kipaumbele kwanza kwa ufanyiaji marekebisho usimamizi, kisha maendeleo endelevu na ufadhili kwa ajili ya maendeleo, mfumo wa usalama, haki za binadamu na ushiriki wa raia, uhamiaji, na kisha, jinsi ya kuyatimiza malengo haya. Inamaanisha kuwa tunahitaji vifaa vinavyofaa, ambavyo ni upatanishi, kuendeleza uamuzi wa pamoja, na ubia”

Iwapo hapataibuka wagombea wengine, basi vikao vya leo vitakuwa ndivyo vya mwisho katika mchakato huu unaoendelea wa uteuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo kufikia sasa wagombea tisa wamewasilisha hoja zao na kujibu maswali kutoka kwa wajumbe wa nchi wanachama.