Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza katika kupambana na msongo wa mawazo huleta faida

Kuwekeza katika kupambana na msongo wa mawazo huleta faida

Ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Afya ulimwenguni WHO imekadiria kwa mara ya kwanza faida za kiuchumi na kiafya zinazotokana na uwekezaji katika kupambana na matatizo ya afya ya akili yanayoenea duniani kote.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti la The Lancet, kila dola inayowekezwa katika kuimarisha matibabu ya msongo wa mawazo na wasiwasi inaleta faida ya dola 4 katika afya bora na uwezo zaidi wa kufanya kazi.

Kwa ujumla matatizo hayo mawili yanagharimu dola trilioni moja kila mwaka duniani.

WHO imesema kwamba watu milioni 615, sawa na asilimia 10 ya watu duniani hukumbwa na matatizo ya kuwa na wasiwasi au msongo wa mawazo, idadi hiyo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 50 kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita.