Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya ukiukwaji wa haki vyaongezeka DRC

Visa vya ukiukwaji wa haki vyaongezeka DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, idadi ya visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu imeongezeka mwezi huu ikilinganishwa na mwezi Februari mwaka huu.

Hii na kwa mujibu wa Jose Maria Aranaz, mkuu wa ofisi ya haki za binadamu nchini humo, aliyewasilisha ripoti yake leo mbele ya waandishi wa habari mjini Kinshasa.

Amesema visa 410 vya ukiukwaji wa haki za binadamu vimeorodheshwa, asilimia 65 vikiwa vimetekelezwa na vikosi vya usalama vya serikali, hasa polisi na wanajeshi. Hata hivyo, amekaribisha hatua za serikali katika kupambana na ukwepaji sheria, akisema askari 14 wa jeshi walihukumiwa mwezi wa Machi kutokana na vitendo vya ukiukwaji wa haki.

Aidha Bwana Aranaz ameelezea wasiwasi wa Ofisi yake kuhusu mivutano ya kikabila kwenye maeneo ya Lubero na Walikale, mashariki mwa nchi.

Kuhusu mchakato wa uchaguzi, amesema visa 46 vimehusishwa na mchakato huo, akiongeza kwamba uchaguzi hautaaminika iwapo wadau wote hawatapewa haki ya kuandamana kwa uhuru.