Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu wa Tisa wa UM waanza

Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu wa Tisa wa UM waanza

Mchakato wa kusaka Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa atakayeshika wadhifa huo baada ya Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon kumaliza n’gwe yake mwishoni mwa mwaka huu, umeanza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Mchakato huo unahusisha mahojiano na wagombea wanaowania kushika wadhifa huo.

Idadi ilikuwa wagombea wanane lakini jioni ya Jumatano Aprili 12 ilitangazwa mgombea mwingine Vuk Jeremic kutoka Serbia. Siku hiyo ya Jumatano mchakato ulianza kwa mashauriano hayo yasiyo rasmi yakiongozwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykettoft. Je nini kilifanyika? Amina Hassan anahabarisha katika makala hii.

Nats..

Ndani ya moja za kumbi za mikutano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Mogens Lykketoft, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akiitisha kikao cha mazungumzo yasiyo rasmi ya kuhoji wagombea nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa…

Nats…

Wagombea wako wanane, lakini Baraza limetenga siku tatu za kuwahoji likianza na watatu siku ya Jumanne Aprili 12…Utaratibu ni mgombea kutoa hotuba tangulizi ya dakika 10…

Nats..

Bwana Mogens akimtambulisha wa kwanza!  Dokta Igor Luksic [LUCHICH] Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa mambo ya kigeni wa Montenegro! Yeye amegusia masuala ya ushirikiano baina ya mataifa, uchumi, amani, na maendeleo na ndipo swali kutoka kwa vijana..

Nats…

Anaulizwa hapa ni vipi atahakikisha nchi zinawajibika kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi?

(Sauti Igor)

“Naamini kwamba hatua tunayopaswa kufanya  sasa ni kuhakiisha tunatia saini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wiki ijayo ili uridhiwe na hatimaye uanze kutekelezwa. Naamini Umoja wa Mataifa una wajibu kwa mashirika yake, naamini mengine yanafanya kazi nzuri sana lakini tunapaswa kuhakikisha tuko pamoja.”

Nats…

Wa pili!... akitambulishwa, Irina Bokova kutoka Bulgaria Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO..hotuba yake ikagusia masuala ya usawa wa kijinsia, maendeleo  na miongoni mwa masuala aliyoulizwa ni utekelezaji wa ajenda 2030, nini jambo la msingi kuzingatia?

(Sauti Irina)

“Tunapaswa kuondokana na mazoea  kuwa ajenda 2030 itatekelezwa kwa kuongeza uhisani au tulivyofanya MDGs. kupitia wahisani tu. Sote tunafahamu ni lazima tubadilike na mabadiliko, ni kuangalia njia mpya za kuchangisha fedha kwa maendeleo. Kuhamasisha rasilimali za maeneo husika na sisi Umoja wa Mataifa kuja na miundo mipya ya utendaji.”

Nats..

Mogens akimtambulisha Antonio Guterres kutoka Ureno ambaye hadi mwaka jana alikuwa Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR). Yeye akamulika migogoro inayosababisha mizozo ya kibinadamu, ikilazimu watu kukimbia makwao, akisisitiza kuwa aghalabu suluhu ni la kisiasa:

(Sauti Guterres)

“Mahali bora zaidi pa kushughulikia mizizi ya taabu ya wanadamu, ni katikati mwa mfumo wa Umoja wa Mataifa, na ndiyo maana ninagombea wadhifa wa Katibu Mkuu. Sote husema, jamii ya kimataifa hutumia muda mwingi na rasilmali kudhibiti mizozo, kuliko kuizuia. Lakini naamini kuzuia ni lazima kuwe siyo tu jambo la kuzingatia, bali  jambo la kipaumbele katika kila tufanyalo.”

Mazungumzo mengine yanaendelea leo Aprili 13, hitimisho likiwa kesho Alhamisi Aprili 14.