Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka ghasia zikomeshwe Congo, atuma mjumbe Brazzaville

Ban ataka ghasia zikomeshwe Congo, atuma mjumbe Brazzaville

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na ripoti kwamba operesheni za vikosi vya usalama vya serikali ya Jamhuri ya Kongo katika jimbo la Pool zimedaiwa kusababisha mashambulizi dhidi ya raia na kuwalazimu watu kukimbia makwao katika maeneo yaliyoathirika.

Ban ameeleza pia kusikitishwa na vizuizi dhidi ya kulifikia jimbo hilo, ambavyo vinatatiza ukusanyaji taarifa, kufanya tathmini, na kuripoti kuhusu hali halisi.

Aidha, Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali ya Congo kuhakikisha kuwa wahudumu wa kibinadamu na wengineo wanawezeshwa kuyafikia maeneo yaliyoathirika, pamoja na raia, na kwamba vikosi vya usalama vinaendesha operesheni zao kwa kuzingatia wajibu wa nchi hiyo chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria ya kibinadamu.

Ban amelaani vitendo vyote vya ghasia na kutoa wito kwa pande zote kujizuia, na kuanza mazungumzo jumuishi baada ya uchaguzi wa rais.

Katibu Mkuu ametuma Mwakilishi wake maalum kuhusu Afrika ya Kati na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika kanda hiyo, Abdoulaye Bathily, kwensa Brazzaville kushauriana na mamlaka za nchi na wadau wengine.