Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM kutathimini hali ya watu wenye ulemavu Zambia

Mtaalamu wa UM kutathimini hali ya watu wenye ulemavu Zambia

Mratibu maalum wa Umoja wa mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu Catalina Devandas-Aguilar atazuru kwa mara ya kwanza Zambia kuanzia April 18 hadi 28 mwaka huu.

Katika ziara hiyo atatathimini hali ya watu wenye ulemavu ikiwemo wazee, wanawake, na watoto pamoja na sheria, sera na mipango iliyowekwa kuhakikisha haki za watu hao.

Bi Devandas-Aguilar amesema katika ziara yake ya siku 10 atajikita zaidi katika suala la haki za watu wenye ulemavu nchini Zambia hasa kwenye nyanja za ulinzi wa kijamii, elimu, afya ya akili, fursa ya haki na kunyimwa uhuru.

Pia amesema wakati huu wa harakati za kabla ya uchaguzi mkuu utaofanyika nchini humo mwezi Agosti mwaka huu, atataka pia kutathimini jinsi gani watu wenye ulemavu wana haki ya ushiriki wa mchakato wa kisiasa na jinsi zinavyoshughulikiwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Atazuru Zambia kwa mwaliko maalum wa serikali ya nchi hiyo, na mbali ya viongozi wa serikali pia atakutana na mashirika ya watu wenye ulemavu, wadau wa jumuiya za kijamii, maafisa wa Umoja wa Mataifa, wahisani wa kimataifa na atazuru miji ya Lusaka na Ndola.