Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvamizi wa nzige wa jangwani Yemen watia hatarini nchi jirani- FAO

Uvamizi wa nzige wa jangwani Yemen watia hatarini nchi jirani- FAO

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), limeonya kuwa uvamizi wa nzige wa jangwani hivi karibuni nchini Yemen, ambako mzozo unavuruga juhudi za kuudhibiti, unazua uwezekano wa tishio kwa mimea katika nchi jirani.

FAO imetoa wito kwa nchi jirani za Saudia, Oman na Iran, kuchagiza timu za kufuatilia na kudhibiti ueneaji wa nzige, na kuchukua hatua zote kuzuia nzige hao kuyafikia maeneo ya kuzalishana ndani ya mipaka yao.

Aidha, FAO imesema nchi za Morocco na Algeria zinapaswa pia kuchukua tahadhari, hususan katika milima ya Atlas, ambayo huenda ikawa maeneo ya kuzalishana kwa nzige wa jangwani waliokusanyika katika maeneo ya Sahara Magharibi, Morocco na Mauritania.

Nzige walianza kukusanyika kwenye pwani ya kusini mwa Yemen mnamo mwezi Machi, kufuatia mvua zilizohusishwa na vimbunga Chapala na Megh, vya Novemba 2015.