Majanga ya muda mrefu lazima yashughulikiwe ili kutimiza Ajenda 2030- WHO

Majanga ya muda mrefu lazima yashughulikiwe ili kutimiza Ajenda 2030- WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema linajizatiti katika utekelezaji wa malengo endelevu, yaani SDG’s, yaliyozinduliwa hivi karibuni na kuhakikisha hakuna atakayesalia nyuma ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, WHO imesema inafanya kazi katika nchi nyingi ambazo zimeathirika na majanga ya muda mrefu , hasa yanayosababishwa na vita, na nchi hizo ndizo zinazokumbwa na vizuizi katika kufikia malengo hayo.

WHO inakadiria kwamba kuna asilimia 60 ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya wajawazito, asilimia 53 ya vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano na asilimia 45 ya vifo vya wakati wa kujifungua vinavyotekea katika mazingira ya vita, watu kutawanywa na majanga ya asili.

Shirika hilo limeongeza kuwa kwa mwaka 2016 WHO ikishirikiana na wadau wengine wanatoa msaada kwa mahitaji ya kiafya katika majanga ya kibinadamu zaidi ya 30.

WHO imesema majanga ya muda mrefu yanaathiri maisha ya watu, uchumi na jamii kwa muda mrefu. Imetoa mfano taifa changa la Sudan Kusini, ambalo shirika hilo linasema linahitaji msaada zaidi kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.