Mchakato wa kumpata mrithi wa Ban waanza leo
Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa atakayechukua nafasi baada ya Ban Ki-moon kuhitimisha muhula wake mwishoni mwa mwaka huu umeanza hii leo jijini New York, Marekani. Grace Kaneiya na Ripoti kamili.
(Taarifa ya Grace)
Mchakato unahusisha mazungumzo yasiyo rasmi na wagombea wote wanane, wakiulizwa maswali kutoka mashirika ya kiraia. Mchakato utaendelea hadi tarehe 14 mwezi huu ambapo leo wanaohojiwa ni watatu ambao ni Dkt. Igor Luksic kutoka Montenegro, Irina Bokova kutoka Bulgaria na Antonio Guterres kutoka Ureno.
Akifungua mchakato huo Rais wa Baraza Kuu la Umoja Mataifa Mogens Lykketoft amesema hii ni mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa uteuzi na uchaguzi kuongozwa kwa misingi ya uwazi na ushirikishi akisema
(Sauti ya Lykketoft)
“Mchakato huu unatoa fursa kwa Baraza kujithibitisha, kuweka viwango vipya vya uwazi na ushirikishi katika michakato ya Umoja wa Mataifa na muhimu zaidi kusaidia kupata mgombea bora atakayekuwa Katibu Mkuu wetu ajaye.”
Mazungumzo hayo yanayoratibiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yataendelea kesho.