Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukizi ya mauaji ya kimbari Rwanda: Ban asema yasitokee tena

Kumbukizi ya mauaji ya kimbari Rwanda: Ban asema yasitokee tena

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amehudhuria kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda iliyofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, akikariri msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha mauaji kama hayo yasitokee tena duniani kote.

Amekumbusha kwamba wengi wa watu 800,000 waliofariki duniani walikuwa ni Watutsi lakini kwamba baadhi ya Wahutu na Watwa wenye msimamo wa kati waliuawa pia.

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mauaji ya kimbari hayatokei ghafla, bali ni mchakato unaochukuwa muda mrefu wa maandalizi, na moja ya ishara za kwanza ni maneno ya chuki yanayosambazwa kupitia vyombo vya habari.

Akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kupambana na mizizi hii ya mauaji, amesema:

(Sauti ya Bwana Ban)

“ Yasitokee tena, tunaendelea kusema. Lakini kila siku duniani kote, wanaume, wanawake na watoto wanaendelea kuuawa, kubakwa, kufurushwa makwao na kunyanyaswa kwa msingi wa asili yao. Tunapaswa kuungana ili kukuza ujumuishi, mazungumzo na utawala wa sheria kwa ajili ya jamii zenye amani.”