Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misri yatakiwa isitishe uvunjifu wa haki za binadamu na mashirika ya kiraia

Misri yatakiwa isitishe uvunjifu wa haki za binadamu na mashirika ya kiraia

Umoja wa Mataifa umeelezea kusikitishwa na kuendelea kuzorota kwa haki za wapigania haki za binadamu na mashirika ya kiraia nchini Misri.

Kupitia taarida ya wataalamu watatu wa haki za binadamu wa UM, wameonya kuwa mashirika mengi nchini humo yamefungwa, watetezi wa haki za binadamu wamehojiwa na vikosi vya usalama, kuzuiwa kusafiri na mali zao kutoweshwa.

Wataalamu hao Michel Forst, David Kaye, Maina Kiai, wamenukuliwa wakisema kuwa Misri imeshindwa kuhakikisha mazingira bora na salama kwa mashirika hayo nchini humo, na kuitaka serikali ikomeshe aina zote za mateso na kuchukua hatua za kulinda mashirika hayo.

Kadhalika wamesisitiza wito wao kwa taifa hilola Kaskazini mwa Afrika kufanya marekebisho ya sheria namba 84/2002 kuhusu mashirika yasiyo ya kiserikali bila kuchelewa ambayo wamesema bado imesalia licha ya kukosolewa pakubwa.