Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la dola Milioni 200 kukwamua Haiti

Ombi la dola Milioni 200 kukwamua Haiti

Umoja wa Mataifa nchini Haiti umetangaza ombi la dola Milioni 200 kukwamua nchi hiyo kutoka mlolongo wa matatizo yanayoikabili.

Habari zinasema miaka sita tangu tetemeko kubwa la ardhi likumbe nchi hiyo, hali ya kibanadamu imeendelea kuzorota, uhakika wa chakula ukisalia ndoto, ugonjwa wa kipindupindu ukiathiri afya za wananchi na ukame nao ukikumba nchi hiyo mwaka wa tatu mfululizo.

Jens Laerke kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu anasema..

(Sauti ya Jens)

"Tunachoshuhudia tangu katikati ya mwaka 2015 ni kuzorota kwa hali ya kibinadamu ambako kumesababisha ombi hili la usaidizi. Kimsingi kinachotokea ni mkusanyiko wa viashiria vya hatari; ukame ambao unaathiri sana wananchi na hii ina maana takribani watu Milioni Moja hawana uhakika wa chakula.”

OCHA imesema pamoja na hali hiyo, watu Elfu 62 bado wanaishi kwenye kambi tangu tetemeko la ardhi mwaka 2010, huku maradufu ya idadi hiyo ni wananchi waliorejeshwa kutoka Dominica ambao nao pia wanahitaji msaada wa kibinadamu.