Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM ataka usiri wa kifedha ukomeshwe

Mtaalam wa UM ataka usiri wa kifedha ukomeshwe

Kufuatia sakata la Panama Papers, Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu deni la kigeni na haki za binadamu, Juan Pablo Bohoslavsky, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa ikomeshe hima usiri wa kifedha ili kumaliza usafirishaji haramu wa fedha. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Bwana Bohoslvasky ameonya kuwa ukwepaji kodi na usambazaji wa fedha ambazo zimepatikana kwa njia haramu hudunisha haki na kuzifanya serikali zikose rasilmali zinazohitajika kwa minajili ya kuendeleza haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Wito wake unafuatia kufichuliwa kwa siri katika hati ambazo zimeonyesha kuwa kampuni, watu tajiri na watu walio na uhusiano wa karibu na wanasiasa, wamekuwa wakificha mali katika akaunti 21 tofauti za nchi za ng’ambo.

Bwana Bohoslavsky amesema ingawa watu wengi huenda walikuwa na nia tofauti katika kuhifadhi fedha na mali zao katika kampuni zaidi ya 21,000 za ng’ambo, huenda ukwepaji kodi, kuficha fedha zilizopatikana kwa njia fisadi na haramu ndiyo hasa sababu kuu ya kufanya hivyo.