Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ziepushe utesaji wa watoto- Zeid

Serikali ziepushe utesaji wa watoto- Zeid

Mfuko wa hiari wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia wahanga wa mateso, UNVFVT leo umezindua kitabu From horror to healing, kinachoonyesha safari ya wahanga wa mateso ikiwemo madhila wanayopata hadi wanapopona.

Uzinduzi huo umefanyika Geneva, Uswisi ambapo Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein ameangazia mateso wanayopata watoto wakimbizi na wahamiaji ikiwemo ukatili wa kingono kutoka kwa wasafirishaji haramu, magenge ya wahalifu na hata mawakala wa serikali akisema..

(Sauti ya Zeid)

“Idadi ya kutisha ya watoto wahamiaji wanateseka mipakani na wanaweza kupata vipigo wakiwa wanashikiliwa na mawakala wa serikali. Ni muhimu sana kwa serikali kulinda haki za wahamiaji wote na zaidi watoto wahamiaji.”

Simulizi katika kitabu hicho zimekusanywa kutoka vituo na mashirika yanayopata msaada wa moja kwa moja kutoka mfuko huo wa hiari kwa ajili ya kusaidia wahanga takribani Elfu Hamsini wa mateso na familia zao kila mwaka.