Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yafungua tena uteuzi wa wagombea wa tuzo ya Nansen

UNHCR yafungua tena uteuzi wa wagombea wa tuzo ya Nansen

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limeitisha tena uteuzi wa wagombea wa tuzo ya Nansen kuhusu wakimbizi kwa mwaka 2016, ambao unafanyika hadi tarehe 25 Aprili.

Tuzo hiyo ya kiutu hutolewa kama heshima kwa mtu au kikundi cha watu ambacho kimeenda hatua zaidi ya kazi yao ya kila siku ili kuwasaidia wakimbizi, watu waliofurushwa makwao au watu wasio na utaifa.

Mshindi wa tuzo hiyo hupewa medali pamoja na dola laki moja za Kimarekani, ambazo hutolewa na serikali za Norway na Switzerland kwa minajili ya kusaidia mradi wowote ule anaochagua mshindi kwa manufaa ya wakimbizi.

Hati za uteuzi utakaofanyika katika kipindi hiki cha Aprili 5 hadi Aprili 25, zitafanyiwa tathmini pamoja na zile za uteuzi uliofungwa mnamo Februari 8 2016, na mshindi kutangazwa mnamo mwezi Septemba 2016.