Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wakimbizi waliopo Ugiriki watendewe haki: UNICEF

Watoto wakimbizi waliopo Ugiriki watendewe haki: UNICEF

Huku utaratibu wa kupeleka Uturuki wakimbizi waliopo Ugiriki ukiwa umeanza kutekelezwa, shirika la Kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF limekumbusha serikali wajibu wao katika kulinda watoto na kuwapatia haki ya kusikilizwa kabla ya kuwasafirisha.

Kauli hiyo imetolewa leo na UNICEF huku ikikaribisha sheria mpya iliyopitishwa na Ugiriki, inayozuia baadhi ya vikundi kurudishwa kwa nguvu, wakiwemo watoto wasioambatana na mzazi au mlezi, wanawake wajawazito, na watoto wenye ulemavu. Wiki hii tayari wakimbizi kadhaa walirudishwa Uturuki kufuatia makubaliano katika ya Uturuki na Muungano wa Ulaya.

Hata hivyo UNICEF imesema juhudi zaidi zinahitajika, huku wakimbizi na wahamiaji 22,000 wakiwa wamekwama Ugiriki, miongoni mwao asilimia 10 wakiwa ni watoto wasioambatana na mzazi au mlezi yeyote.

UNICEF imeongeza kwamba utaratibu huo wa kuwasafirisha unapaswa kuendeshwa vizuri na kwa kuheshimu mahitaji na haki za watoto, huku ikisikitishwa na kufungwa kwa baadhi wa watoto Ugiriki, sehemu za kuwapa hifadhi zikiwa zimejaa.