Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari za athari za mabadiliko ya tabianchi hazipaati kipaumbele- IFAD

Habari za athari za mabadiliko ya tabianchi hazipaati kipaumbele- IFAD

Ripoti mpya ya utafiti uliofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), imebaini kuwa huku watu milioni 60 duniani wakikabiliwa na njaa kali kwa sababu ya El Niño, na mamilioni ya wengine wakiathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, vyombo mashuhuri vya habari Ulaya na Marekani vinapuuza kutoa kipaumbele kwa habari za masuala hayo.

Akizindua ripoti hiyo, Rais wa IFAD, Kanayo F. Nwanze, amesema inastaajabisha kuwa katika mwaka ambapo kumekuwa na viwango vya joto vilivyoweka rekodi mpya, matukio 32 ya ukame, na hasara kubwa ya mimea, vyombo vya habari haviweki habari za mabadiliko ya tabianchi kwenye kurasa za mbele za machapisho yao.

Amesema mabadiliko ya tabianchi ndilo tishio kubwa zaidi linaloikabili dunia sasa, na jinsi vyombo vya habari vinavyolishughulikia suala hilo ni muhimu sana katika kukabiliana na mizozo ya tabianchi katika siku zijazo.

Ripoti hiyo: “Hadithi isiyosimuliwa: Mabadiliko ya tabianchi yasukumwa chini ya vichwa vya habari” inatoa tathmini ya kina kuhusu jinsi vyombo vya habari duniani vinavyoripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika nyakati mbili tofauti, ambazo ni miezi miwili kabla ya kongamano la 21 kuhusu tabianchi (COP21), jijini Paris, mwezi Disemba 2015, na miezi miwili baada ya kongamano hilo.