Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yalaani shambulio kwenye hospital ya Ma’arib-Yemen

WHO yalaani shambulio kwenye hospital ya Ma’arib-Yemen

Shirika la afya duniani WHO limelaani vikali shambulio kwenye hospitali kuu ya Ma’arib iliyoko kwenye jimbo la Ma’arib nchini Yemeni na kukatili maisha ya watu wanne akiwemo Daktari wa hospitali hiyo na pia kujeruhi watu wengine 13 mnamo Aprili 3 mwaka huu.

Shambulio hilo pia limesababisha uharibifu mkubwa kwenye kitengo cha wagonjwa mahtuti jengo la idara ya uongozi wa hospitali hiyo.

Licha ya kukabiliwa na upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya na madawa, hospitali ya Ma’arib inatoa huduma ya afya inayohitajika haraka na maelfu ya watu wa eneo hilo na majimbo mengine ikiwa ni pamoja na majimbo ya Al-Jawf, Al-Baidha'a, Aden na Lahj.

Kwa mara nyingine WHO imetoa wito kwa pande hasimu katika mgogoro wa Yemen kuheshimu usalama na wahudumu wa afya na vituo vya afya na kusistiza kwamba mashambulio kama haya moja kwa moja yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.