Skip to main content

Walinda amani wa DRC wanaodaiwa kubaka CAR mahakamani

Walinda amani wa DRC wanaodaiwa kubaka CAR mahakamani

Kesi dhidi ya watu 20 waliokuwa walinda amani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR imeanza wiki hii mjini Kinshasa.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na redio ya Umoja wa Mataifa nchini DRC Radio Okapi.

Radio Okapi inaeleza kwamba baadhi ya watu hao wanatuhumiwa kubaka wasichana wenye umri wa chini ya miaka 18. Wengine wanashukiwa kuwa wamepinga uamuzi wa uongozi wao, huku baadhi yao wakituhumiwa kuondoka kambini bila kuruhisiwa na kujumuika na raia wa Bangui.

Kuhusu kesi za ubakaji, wakili wa jeshi la kitaifa FARDC amesisitiza kwamba hakuna ushaihidi wa kutosha.

Walinda amani 108 wa DRC waliokuwa wakitumikia CAR kama kikosi cha polisi wamerudishwa kwao mwezi Januari mwaka huu baada ya kumaliza majukumu yao nchini humo. Kikosi hicho kilitumwa CAR tangu mwanzo wa mzozo Disemba mwaka 2013.