Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wataka uchunguzi kuhusu vifo katika kituo cha kuzuilia wahamiaji Libya

UM wataka uchunguzi kuhusu vifo katika kituo cha kuzuilia wahamiaji Libya

Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mratibu mkaazi wa masuala ya kibinadamu nchini Libya, Ali-Za’tari, ameelezea masikitiko yake kufuatia vifo vya wahamiaji wanne kutoka Kusini mwa Jangwa la Afrika katika kituo cha kuzuilia wahamiaji cha Al-Nasr, huko al-Zawiya, na kutoa wito uchunguzi kamili ulio huru na wa haki, ufanyike kuhusu vifo hivyo.

Aidha, mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu amewatakia uponaji haraka wahamiaji waliojeruhiwa na mlinzi mmoja.

Kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Libya, UNSMIL, wafungwa wanne waliuawa kwa kupigwa risasi, na wengine 20 wakajeruhiwa wakati wa, na baada ya jaribio la kuitoroka kituo cha kuzuilia “wahamiaji haramu” cha Al-Nasr mnamo Aprili mosi.

Imeripotiwa pia kuwa mazingira katika kambi hiyo si yenye utu, kukiwa na msongamano mkubwa, uhaba wa chakula na vifaa vingine vya msingi, na kutopatikana huduma ya afya.