Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia mizozo ndio msingi kwa usalama wa kimataifa- Eliasson

Kuzuia mizozo ndio msingi kwa usalama wa kimataifa- Eliasson

Ni lazima kukabiliana na mizizi ya mizozo, amekariri leo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, akihutubia mkutano wa tano wa mazungumzo ya kimataifa kuhusu ujenzi wa amani na taifa, mjini Stockholm, Sweden.

Bwana Eliasson amesema, wakati ambapo dunia inakumbwa na hatari nyingi zaidi kutokana na ugaidi, udhaifu wa serikali, ukosefu wa usawa na ajira kwa vijana, ni muhimu zaidi kuzuia mizozo, akisema ndio msingi katika kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Akiongeza kwamba hakuna suluhu ya moja kwa moja kwa ajali ya kujenga amani na taasisi za serikali kwenye nchi zilizo katika hali tete, amesisitizia mazungumzo jumuishi ya kisiasa, ushirikiano, na uwekezaji zaidi wa mashirika ya kimataifa.

Bwana Eliasson amesikitishwa kwamba mfuko wa ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa amani unafadhili kwa kiasi cha dola milioni 100 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya misaada ya kibinadamu ambayo ni dola bilioni 20.

Miongoni mwa harakati zinazochukuliwa na mkutano huo unaofanyika nchini Sweden ni uwekezaji katika mfumo uitwao New Deal kwa ajili ya kukwamua nchi zilizodhoofika na hivyo kuzuia mizozo.