Skip to main content

ICC yatupilia mbali kesi dhidi ya Ruto na Sang

ICC yatupilia mbali kesi dhidi ya Ruto na Sang

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, huko The Hague, Uholanzi imetupilia mbali kesi dhidi ya William Ruto na Joshua arap Sang.

Uamuzi wa kufuta kesi hiyo umefuatia ombi la wawili hao la mwezi Oktoba mwaka jana kukubaliwa na majaji wawili kati ya watatu waliokuwa wanaounda jopo linalosikiliza kesi hiyo.

Majaji waliounga mkono ombi la kesi kufutwa na kwamba hakuna kesi ya kujibu ni Chile Eboe-Osuji na Robert Femr ambapo jaji wa tatu Olga Herrera Carbuccia  alipinga lakini hoja ya wengi wape ikawezesha ombi la washtakiwa kushinda.

Fadi El Abdallah ni msemaji wa ICC na alizungumza baada ya uamuzi kutolewa..

(Sauti ya Fadi)

“Mahakama ya ICC ya 5(A), imeaamua kwa wingi, huku Jaji Herrera-Carbuccia akipinga, kwamba kesi dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang ifutiliwe mbali. Kulingana na uamuzi wa wengi, uamuzi huu hautozuia kufunguliwa kwa mashtaka mapya siku zijazo, iwe katika ICC au katika mahakama ya kitaifa. Uamuzi huu unaweza kukabiliwa na ombi la rufaa. Mahakama ilizingatia maombi ya Bwana Ruto na Bwana Sang, ya kutaka iamue kuwa hakuna kesi ya kujibu, ifutilie mbali mashtaka dhidi ya washukiwa wote, na kutoa hukumu ya kutokuwa na hatia. Mahakama pia ilizingatia maelezo ya kupinga maombi hayo kutoka kwa Mwendesha Mashtaka na mawakili wa wahanga, na ikapokea maoni mengine yaliyowasilishwa wakati wa kikao kilichofanyika kutoka tarehe 12 hadi 15 Januari 2016. 

Majaji waliokubali ombi la kufutwa kesi walitoa sababu mbali mbali mathalani Jaji Femr alisema hakuna kesi ya kujibu kwa kuzingatia tathmini ya ushahidi wa upande wa mashtaka kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama tarehe Tatu mwezi Juni mwaka 2014.

Kwa upande wake Jaji Herrera Carbuccia alisema uamuzi wake wa kupinga unazingatia kuwa upande wa mashtaka haujasambaratika na kuna ushahidi wa kutosha iwapo utakubalika kwa kesi kusikilizwa.

Ruto na Sang walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Kenya  ikiwemo mauaji, kuwafurusha watu makwao au kuwatoa watu makwao bila hiari yao na mateso.

Makosa hayo yadaiwa kufanyika mwaka wa 2007 na 2008 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.